Je, kwa nini Mohammed Badie alikamatwa?
Badie, kiongozi wa kundi la Muslim Brotherhood, anajulikana kama "mtu aliye nyuma ya Morsi", ikimaanisha kuwa, ana uwezo wa kumdhibiti Morsi na pia, yeye ndiye anayetoa maamuzi halisi ya masuala mbalimbali ya Misri. Tangu Morsi aondolewe madarakani na jeshi mwezi uliopita, maandamano na vurugu vimetokea kwenye sehemu nyingi nchini humo na kusababisha vifo na majeruhi ya watu wengi. Idara ya uendeshaji mashtaka ilitoa amri ya kumkamata Badie tarehe 10 Julai kwa tuhuma za kuhusika na kuchochea mauaji dhidi ya wapinzani wa Morsi.
Baada ya hapo, Badie alijitokeza hadharani mara kadhaa akiwahamasisha wafuasi "kulinda uhalali wa Morsi kwa damu", na wanachama wa kundi hilo na wafuasi wa Morsi wakaanza maandamano, na hata kufanya mashambulizi dhidi ya idara za polisi, makanisa na miundombinu ya umma. Kwa hiyo Badie anachukiwa zaidi na jeshi na polisi nchini Misri. Hatma ya Muslim Brotherhood kufuatia kukamatwa kwa Badie
Kabla ya kukamatwa kwa Badie, serikali ya Misri iliwataja baadhi ya wanachama wa kundi la Muslim Brotherhood kuwa ni magaidi, na waziri mkuu wa nchi hiyo Hazem el-Beblawi, alitoa pendekezo rasmi la kuvunja kundi hilo kwa mujibu wa sheria. Ikulu ya Misri pia ilitangaza kuwa nchi hiyo inakabiliwa na "vita iliyozushwa na magaidi", na kusisitiza nia thabiti ya kupambana na ugaidi. Hivyo kundi la Muslim Brotherhood lilikabiliwa na shinikizo la kuvunjwa na kuangamizwa kwa nguvu ya kijeshi, zaidi ya hayo, kukamatwa kwa Badie sasa kumeondoa uongozi wa kundi hilo, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa kundi hilo.
Wachambuzi wanaona kuwa, serikali ya Misri itaendelea kuchukua hatua dhidi ya viongozi waandamizi wengine wa kundi hilo, huenda itavunja kundi hilo baada ya kumaliza utaratibu husika wa kisheria. Kwa sasa mustakbali wa kisiasa wa kundi hilo ni mbaya, na huenda litaondolewa kabisa kwenye uwanja wa siasa nchini humo. Lakini Muslim Brotherhood, likiwa ni kundi lenye nguvu kubwa wa kidini na historia ya miaka zaidi ya 80, bado lina nguvu kubwa ya ushawishi. Athari ya kukamatwa kwa Badie kwa hali nchini Misri
Kukamatwa kwa Badie kutakuwa na athari kubwa kwa kundi la Muslim Brotherhood na hali ya kisiasa ya Misri kwa ujumla. Mambo mbalimbali yanaweza kutokea, kwa mfano, huenda kundi hilo litalipiza kisasi na kuchochea maandamano na vurugu zaidi; au baadhi ya wanachama wenye msimamo wa kati wa kundi hilo huenda wataacha matumizi ya nguvu na kujitahidi kuwasiliana na serikali ili kutimiza maafikiano; pia inawezekana kuwa viongozi wengi wa kundi hilo watakimbilia nje ya nchi; wanachama wa kawaida wa kundi hilo na wafuasi wa Morsi huenda watapunguza maandamano na kutathmini upya hali ya nchi hiyo.
Baada ya kukamatwa kwa Badie, huenda vurugu na matukio ya kimabavu yataongezeka kwa muda mfupi na kuwa mabaya zaidi. lakini kundi la Muslim Brotherhood litapoteza, hatua kwa hatua, nguvu ya kuhamasisha mamilioni ya watu kufanya maandamano. Misri inatazamiwa kurejea kwenye hali ya kawaida kutokana na juhudi za serikali na jeshi.